Mgogoro wa uwanja wa Kanisa la Gofan na Jiji umechukua sura mpya baada ya Kanisa hilo kugoma kwenda mahakamani kama walivyoshauriwa na Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson Kanisa likidai mgogoro ulikwisha.
Kikao cha mwisho kilichofanyika hivi karibuni ambacho kilihudhuriwa na Dkt Tulia Ackson na kuzisikiliza pande zote ambapo alilishauri Kanisa kwenda mahakamani ili Kanisa liweze kupata haki yake.
Siku chache baada ya ushauri huo Mchungaji John Ikowelo na waumini wake wamejitokeza kufanya usafi eneo linalogombaniwa ambapo Mchungaji amesema yeye hawezi kuishitaki serikali kwani serikali imemfanyia mambo mengi na ilimaliza kabisa mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka kumi.
Nao baadhi ya waumini wamesema mgogoro umekwisha wanachosubiria ni kibali cha ujenzi ambacho Jiji wanasita kuwapatia kwa muda mrefu hivyo wameamua kufanya usafi kwenye uwanja wao ikiwa ni maandalizi ya ujenzi wa Kanisa.
Mgogoro umedumu kwa zaidi ya miaka kumi ambapo kila upande unadai hilo ni eneo lake Jiji wakidai ni la shule ni eneo oevu halipaswi kujengwa nyumba huku Kanisa likidai eneo ni halali yao.