Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amefungua rasmi Kongamano la nne la Afrika la Uhifadhi wa Biolojia lililowakutanisha wataalamu wabobezi takribani 300 kutoka nchi mbalimbali Barani Afrika na nje ya Bara la Afrika lengo ikiwa ni kuendeleza uhifadhi wa maliasili na Bioanuwai.
Ufunguzi huo umefanyika katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka (College of African Wildlife Management- CAWM), Moshi Mkoani Kilimanjaro leo Oktoba 19,2024.
“Tunahitaji uhifadhi endelevu kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye kwani uhifadhi ni ajira, unaongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla kutokana na mapato na kuingiza fedha za kigeni, hivyo ajenda kuu ya kongamano hili ni uhifadhi” amesisitiza Mhe. Chana.
Amefafanua kuwa mojawapo ya masuala yatakayojadiliwa katika kongamano hilo ni wajibu wa Askari Uhifadhi na jamii katika kuendeleza uhifadhi barani Afrika, kulinda Bioanuwai katika Mabadiliko ya Tabia Nchi, Biolojia ya uhifadhi na kujenga uwezo na mafunzo ya uhifadhi Barani Afrika.
Ametumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kuwajibika kuhakikisha masuala ya uhifadhi yanapewa kipaumbele huku akisisitiza kuwa Kongamano hilo limefanyika katika chuo hicho ikiwa ni sehemu ya kuthamini mchango wake kama Kituo cha Ubora cha Mafunzo ya Wanyamapori Mashariki na Kusini mwa Afrika.
“Hadi leo, Chuo kimetoa mafunzo kwa wahitimu zaidi ya 11,000 kutoka nchi 28 za Afrika na 26 za nje ya nchi tangu kilipoanzishwa mwaka 1963” amesisitiza Mhe. Chana.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya MWEKA, Prof. Yunus Mgaya amesema Kongamano hilo ni fursa ya kujadiliana na kubadilishana uzoefu, ujuzi, mafanikio na changamoto zilizopo katika sekta ya uhifadhi.
“Kwa pamoja tutaweza kutengeneza njia sahihi kuelekea uhifadhi endelevu” amesema.
Kongamano hilo la siku tatu lenye kauli mbiu “Kuadhimisha mashujaa wasioimbwa sana na walio mstari wa mbele katika uhifadhi wa Afrika: Askari Uhifadhi na jumuiya za Jamii “limeshirikisha washiriki kutoka nchi za Sweden, Namibia, Uganda, United States, United Kingdom, Uhispania, Australia, Zambia, Nigeria, Kenya, Tanzania n.k
Na Happiness Shayo – Moshi