Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb), ametaja mambo makubwa aliyoyafanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha Sekta ya Maliasili na Utalii.
Ameyasema hayo leo Septemba 24, 2024 alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Peramiho, Mkoani Ruvuma.
Mhe. Chana amesema kuwa Rais ameifungua dunia kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko nchini Tanzania kupitia filamu yake ya “Tanzania the Royal Tour “ sambamba na kuielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kufungua Utalii Kusini.
Ametumia fursa hiyo kuwahamasisha Watanzania kuitazama filamu hiyo na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyoko nchini ikiwamo Makumbusho Maalum ya Majimaji iliyopo mjini Songea Mkoani Ruvuma.
Aidha, Mhe. Chana ameongeza kuwa katika kuhakikisha misitu inalindwa na kuhifadhiwa Rais Samia aliunda Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ili kuhakikisha inashirikiana na Watanzania kuilinda misitu ili kusiwe na jangwa.
Pia, amesema Rais Samia ameweka Idara ya Misitu na Nyuki kwa lengo la kusimamia rasilimali za misitu na nyuki ambapo ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kufuga nyuki na kupanda miti ili kujiinua kiuchumi na kuhifadhi mazingira.