Jopo la Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi 50 kutoka Hospitali za Rufaa na Kanda ya Kusini wanaounda Kambi Rasmi ya Madaktari Bingwa wa Daktari Samia wamepiga Kambi katika Hospitali ya Rufaa ya Sokoine na kutoa huduma za afya za kibingwa kuanzia Jumatatu, Mei 06, hadi Ijumaa Mei 10, 2024.
Akitoa tathmini ya kambi hiyo wakati wa ufunguzi rasmi, Daktari Alexander Makalla, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine ameeleza kuwa Madaktari bingwa na bobezi hao wanatoka katika Hospitali mbalimbali zilizopo nchini ikiwemo hospitali za Rufaa ya Sokoine RRH, Ligula RRH, hospitali za rufaa za Mkoa wa Dar es Salaam kama Amana, Mwananyamala na Hospitali ya Kanda ya Kusini-Mtwara kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanasogezewa huduma za afya za kibingwa katika maeneo yao hivyo kupunguza gharama na adha nyinginezo walizokuwa wanakumbana nazo.
Mhe. Shaibu Ndemanga, Mgeni rasmi katika uzinduzi rasmi wa kambi ya madaktari bingwa wa Daktari Samia amesifu na kutoa shukrani za dhati kwa Serikali ya awamu ya sita chini yake Daktari Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada za kuhakikisha huduma za afya hususani za kibingwa zinasogezwa na zinawafikia wananchi na wahitaji katika maeneo yao.
“Ili kuwafikia wananchi wengi na kuboresha huduma za afya, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Sokoine- Lindi itatoa huduma ya kumuona daktari bingwa bure kwa wagonjwa wasio na bima ambapo watahitajika kuchangia kiasi kidogo kama atahitajika kupata huduma nyingine ikiwemo vipimo, upasuaji na dawa, kwa mgonjwa anaetumia bima basi ataendelea kupata matibabu kwa kutumia bima yake” Mhe. Ndemanga.
Aidha, Mhe. Ndemanga ameeleza kwa kuzingatia kauli ya Mtu ni Afya, serikali itaendelea kuboresha huduma za afya na kuboresha miundombinu ya utoaji huduma za afya kwa kuongeza vituo vya kutolea huduma za afya, ununuzi wa madawa na vifaa tiba ili kuendelea kuboresha na kuwekeza katika afya ya wananchi.