Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dkt. Godlove Mbwanji, kwa kushirikiana na Makamu wa Rais wa taasisi ya Smile Train Afrika, Bi. Nkeiruka Obi, leo Agosti 1, 2025, wamezindua rasmi chumba cha upasuaji kwa watoto kilichokarabatiwa na kuwekewa vifaa vya kisasa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Mbwanji amesema chumba hicho kina mazingira rafiki na ya kuvutia kwa watoto, hatua itakayosaidia kupunguza hofu na kuongeza furaha kwa watoto wanaohitaji huduma za upasuaji.
Kwa upande wake, Bi. Obi amesema Smile Train imekuwa ikitoa huduma nchini tangu mwaka 2006, ambapo zaidi ya watoto 15,000 wamenufaika na mafunzo kutolewa kwa zaidi ya wahudumu wa afya 1,000.
Dkt. Amosi Zakaria, Daktari Bingwa wa Usingizi kwa watoto, ameishukuru Smile Train kwa kufanikisha ukarabati huo na kusema sasa wanaweza kufanya upasuaji mkubwa kwa watoto wa umri wowote.
Tangu kukamilika kwa ukarabati huo, tayari watoto 210 wamefanyiwa upasuaji.