Mgombea Udiwani Kata ya Chokaa Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya Joshua Mlambalala amefikisha maombi ya minara ya mawasiliano kwa Kijiji cha Mapogolo Kata ya Chokaa mbele ya Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi Mbunge mteule wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya kutokana na umuhimu mkubwa kibiashara hasa Wachimbaji wa madini ya dhahabu eneo hilo.
Mlambalala amefikisha kilio hicho kwenye kampeni za Urais, Ubunge na Udiwani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) zilizofanyika Kata ya Chokaa mgeni rasmi akiwa ni Mhandisi Maryprisca Mahundi.
Akijibu maombi hayo Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema suala hilo lipo ndani ya uwezo wake hivyo anawaagiza wataalam haraka iwezekanavyo ili kuwaondolea kadhia wananchi wa Mapogolo.
Akiomba kura Urais, Ubunge na Udiwani Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya maendeleo makubwa hivyo kuna kila sababu ya kukipa kura Chama Cha Mapinduzi.
Aidha amesema wananchi wajitokeze kupiga kura kumchagua Masache Kasaka nafasi ya Ubunge na Joshua Mlambalala nafasi ya Udiwani ili kutimiza mafiga matatu kwa maendeleo ya Kata,Wilaya na nchi kwa ujumla.
Uchaguzi mkuu utatamatisha oktoba 29 mwaka huu ambapo Mhandisi Maryprisca Mahundi ameendelea kuomba kura maeneo mbalimbali nchini.