Mbeya, Septemba 28, 2025 – Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikisha operesheni maalum iliyopelekea kuuawa kwa watuhumiwa waliodaiwa kuhusika na utekaji na mauaji ya kikatili ya Shyrose Michael Mabula [21], mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Mzumbe Ndaki ya Mbeya, Kitivo cha Sheria.
Shyrose aliripotiwa kutekwa nyara Septemba 14, 2025 na mwili wake kupatikana Septemba 16 usiku katika Mtaa wa Morovian, Kata ya Isyesye Jijini Mbeya ukiwa umechomwa moto. Uchunguzi uliofanywa na Polisi uliwakamata watuhumiwa watatu: Marwa Nyahega John [25], Edward Christopher Kayuni, na Websta William Mwantebele [27], ambao walikiri kupanga njama za kumteka kwa lengo la kujipatia fedha kutoka kwa baba yake, Dkt. Mabula Michael.
Kwa mujibu wa Polisi, baada ya kushindikana kwa mpango huo, walimnywesha sumu ya kuulia magugu aina ya Round Up bila mafanikio, kisha wakamnynonga kwa kamba na kuuchoma moto mwili wake.
Mnamo Septemba 27, 2025, wakati wa operesheni katika Kijiji cha Chalangwa, wilayani Chunya, watuhumiwa Edward na Websta walijaribu kukimbia na kuwashambulia askari kwa kisu. Polisi walifyatua risasi za tahadhari, lakini walipokaidi amri, walijeruhiwa kwa risasi na kufariki dunia wakipelekwa hospitalini. Mtuhumiwa wa tatu, Marwa, naye alifariki baada ya kujirusha kutoka kwenye gari la Polisi wakati akipelekwa kuonyesha vielelezo.
Katika upekuzi, Polisi walipata pingu mbili, vitambulisho feki vya JWTZ, simu zenye picha za utekaji na mawasiliano yao, pamoja na taarifa kwamba kidole na nguo za marehemu vilikuwa vimepelekwa kwa mganga wa jadi kwa ajili ya zindiko. Mganga huyo kwa sasa anatafutwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeonya vijana na wananchi kwa ujumla kuacha tamaa ya mali kwa njia za haramu, na kusisitiza kuwa uhalifu haulipi na mkono wa sheria utawafikia popote pale.
Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya