Wadau wa kilimo kutoka taasisi za Serikali na sekta binafsi wamepatiwa mafunzo juu ya matumizi ya mashine za kisasa za kukaushia na kupima unyevu wa mazao ya nafaka, katika warsha iliyoandaliwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na JICA jijini Mbeya.
Warsha hiyo imefanyika tarehe 26 Novemba 2025 katika shamba la Raphael Group Ltd, ambapo mashine ya Batch Circulating Dryer yenye uwezo wa kukaushia hadi tani 8 za mpunga ndani ya saa 4 imeoneshwa kwa vitendo. Teknolojia hii inatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mhandisi Sekela Mwakihaba kutoka Idara ya Zana za Kilimo na Uongezaji Thamani alisema ushiriki wa wadau unaonesha dhamira ya Serikali ya awamu ya sita kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao na kupunguza uharibifu wa nafaka wakati wa uvunaji. Alibainisha pia kuwa Serikali inaendelea kusukuma matumizi ya teknolojia kupitia utekelezaji wa Agenda 10/30 ili kuongeza tija na kipato cha wakulima.
Kwa upande wake, Meneja wa Uzalishaji wa Raphael Group Ltd – Kituo cha Uyole, Bw. Maisha Ambangile, alisema mashine hiyo itasaidia wakulima kupata nafaka kavu kwa ubora wa soko na kwa muda mfupi, huku gharama ya mashine moja ikiwa takriban shilingi milioni 188.
Warsha hiyo imeratibiwa na JICA kwa kushirikiana na kampuni za YAMAMOTO (watengenezaji wa mashine za kukaushia nafaka) na Kett Electric Laboratory (watengenezaji wa mashine za kupima unyevu), ikiwakutanisha maafisa wa Serikali, wataalamu wa JICA, wamiliki wa mitambo ya ukavu na wakulima kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya.

