Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWSA), ikiongozwa na Mwenyekiti wake Bi. Edna Mwaigomole, leo tarehe 03/12/2025 imefanya kikao cha dharula cha Kamati ya Bodi ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kupokea na kujadili Mpango Mkakati wa Mamlaka wa mwaka 2025/2026–2029/2030 na Mpango wa Biashara wa mwaka 2025/2026–2029/2030.
Pamoja na kujadili masuala mengine ya kiutendaji ya Mamlaka, Kamati imepokea taarifa ya ununuzi wa gari maalumu kwa ajili ya shughuli za uondoshaji wa majitaka kwa wateja ambao hawajajiunga na mtandao wa majitaka.
Akitoa taarifa hiyo, CPA. Gilbert Kayange Mkurugenzi Mtendaji wa Mbeya UWSA amesema, Mamlaka ina jukumu la kutoa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa Wananchi ambapo kwa upande wa usafi wa mazingira Mamlaka ilikuwa haijawafikia wateja ambao hawajajiunga katika mfumo rasmi wa majitaka. Hivyo ununuzi wa gari la kuondosha majitaka majumbani utaboresha hali ya usafi wa mazingira katika jamii.
Aidha, alieleza kuwa, Mamlaka imenunua gari aina ya Isuzu FVR34P lenye thamani ya Shilingi 497,000,400 ambalo lina uwezo wa kubeba maji lita 10,000.
Bi. Cynthia Hilda Ngoye Mwenyekiti wa Kamati ya Bodi ya Fedha na Mipango , ameeleza kuwa anafurahishwa na utendaji kazi wa Menejimenti na Watumishi wa Mamlaka kwani mipango mingi inayowekwa inatekelezwa.
Akizindua gari hilo, Bi. Edna ameeleza kuwa fedha zilizotumika kununua gari hilo ni fedha za umma, hivyo ni wajibu wa Watumishi kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Mbeya UWSA inaendelea kutekeleza maboresho ya huduma kwa lengo la kuongeza ufanisi, usalama wa mazingira na ustawi wa wananchi wa Jiji la Mbeya na Mji wa Mbalizi.

