Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Bi. Erica Yegella, leo tarehe 29 Januari 2026 amekutana na waandishi wa habari na kutoa taarifa ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha siku 100, ndani ya Halmashauri hiyo.
Mkutano huo umefanyika katika Ofisi za Mbeya Press Club, eneo la Sokoine Jijini Mbeya, ukiwa na lengo la kuujulisha umma kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uboreshaji wa huduma za kijamii na kiuchumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
Fedha Zilizopokelewa Ndani ya Siku 100
Bi. Yegella amesema kuwa kwa kipindi cha Oktoba 2025 hadi Februari 2026, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imepokea jumla ya Shilingi bilioni 43.7 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 38.4 zimetoka Serikali Kuu, zaidi ya Shilingi milioni 767 kutoka kwa wadau wa maendeleo, huku zaidi ya Shilingi bilioni 4.5 zikitokana na mapato ya ndani ya Halmashauri.
Fedha hizo zimetumika kulipa mishahara ya watumishi wa umma, kuimarisha elimu bila malipo, kuboresha huduma za afya, kuendesha shughuli za kiutawala pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ngazi ya jamii.
Sekta ya Afya
Katika sekta ya afya, Bi. Yegella amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma kwa wananchi kwa kujenga na kukamilisha vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri.
Ameeleza kuwa zaidi ya Shilingi bilioni 1.6 zimetumika katika ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kimkakati Isuto, ukamilishaji wa vituo vya afya vya Ulenje, Mbalizi na Swaya, pamoja na ukamilishaji wa zahanati tisa katika vijiji mbalimbali. Aidha, Halmashauri imenunua vifaa tiba kwa Hospitali ya Wilaya, vituo vya afya na zahanati mpya.
Kwa kipindi cha siku 100, zahanati sita zimefunguliwa rasmi na zinaendelea kutoa huduma, huku zahanati nyingine saba zikiwa katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Sekta ya Elimu
Katika sekta ya elimu, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha sera ya elimu bila malipo kwa kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari.
Bi. Yegella amesema zaidi ya Shilingi bilioni 2.8 zimetumika katika ujenzi wa shule mpya ya elimu ya awali na msingi, ukamilishaji wa maabara za fizikia katika shule za sekondari, ujenzi wa vyoo, madarasa mapya na ukarabati wa shule za msingi. Aidha, madawati 500 yametengenezwa na kusambazwa katika shule 20 za msingi.

Kutokana na jitihada hizo, Halmashauri imeshuhudia ongezeko la vyumba vya madarasa, madawati, matundu ya vyoo pamoja na nyumba za watumishi wa elimu.
Sekta ya Utawala
Kwa upande wa utawala, Bi. Yegella amesema Serikali imepokea zaidi ya Shilingi bilioni 28.4 kwa ajili ya kulipa mishahara ya watumishi zaidi ya 3,600, kuboresha mazingira ya kazi pamoja na kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Katika kipindi hicho, Halmashauri imeajiri watumishi wapya 114 katika kada mbalimbali ikiwemo afya, elimu na utawala, hatua iliyosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Maendeleo ya Jamii
Katika eneo la maendeleo ya jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imeendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kiuchumi.
Bi. Yegella amesema jumla ya Shilingi milioni 485.7 zimetolewa kwa vikundi 15 vyenye wanufaika 108, huku vikundi vingine vikiendelea kupatiwa mikopo katika awamu zinazofuata.
Sekta ya Kilimo na Mifugo
Katika sekta ya kilimo na mifugo, Serikali imeendelea kusajili wakulima kwenye mfumo wa mbolea za ruzuku ambapo zaidi ya wakulima 91,000 wameshasajiliwa. Aidha, tani zaidi ya 13,000 za mbolea za ruzuku zimetumika katika uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Halmashauri pia imezalisha na kugawa bure miche bora 317,000 ya kahawa pamoja na mbegu bora za ufuta kwa wakulima, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji na kipato cha wananchi. 
Hitimisho
Akihitimisha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Bi. Erica Yegella, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuipatia Halmashauri fedha za miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (2025–2030) kwa maslahi ya wananchi.

