Diwani wa Kata ya Utengule Usangu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Ismail Matipa, ametoa sare za shule kwa wanafunzi 400 waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza, katika Shule ya Sekondari Utengule Usangu.
Hatua hiyo imelenga kuondoa changamoto ya baadhi ya wazazi kuchelewesha au kushindwa kuwapeleka watoto wao shule pindi msimu wa masomo unapoanza, hali inayosababishwa na ukosefu wa sare za shule.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Diwani Matipa amesema utoaji wa sare hizo ni sehemu ya jitihada zake za kuunga mkono elimu na kuhakikisha wanafunzi wote wanaanza masomo kwa wakati bila vikwazo vya kiuchumi.
Ameeleza kuwa tukio hilo limefanyika katika wiki ya maadhimisho ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutimiza miaka 49 tangu kuzaliwa kwake mwaka 1977, ikiwa ni ishara ya kuenzi mchango wa chama hicho katika maendeleo ya elimu na ustawi wa jamii.

