Author: admin

*DKT. TULIA AMUOMBA RAIS SAMIA KUBORESHA MIUNDOMBINU JIJINI MBEYA*

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameiomba Serikali kupitia kwa Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuboresha barabara chakavu za mitaa ya Jimbo hilo ambazo ni zaidi ya km 400.

Dkt. Tulia ameyasema hayo wakati wa kilele cha Maonesho na sherehe za wakulima nanenane kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya leo tarehe 8 Agosti, 2023.

Pamoja na ombi hilo, Dkt. Tulia amemshukuru Rais Dkt. Samia na Serikali yake ya awamu ya sita kwa kufanikisha uboreshwaji wa sekta mbalimbali katika Jiji hilo ikiwemo elimu, afya na zaidi kutoa Shilingi Trilioni 1.1 kwa ajili ya kujenga barabara ya njia nne kutokea Igawa hadi Tunduma yenye urefu wa KM 218.

Kuhusu uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Dkt. Tulia amemueleza Rais Dkt. Samia kwamba Wananchi wa Jiji la Mbeya wamemuagiza amueleze kwamba wameukubali na kuubariki uwekezaji huo wenye maslahi mapana kwa taifa.

Akijibu ombi hilo, Rais Dkt. Samia ameahidi kwenda kujipanga na Serikali yake ili kuona namna ambayo wataweza kufanya maboresho hayo ya barabara za mitaa ya Jiji hilo.

Read More

MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO AZINDUA HUDUMA YA MASHINE YA MRI HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA MBEYA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema serikali ya awamu ya sita ina dhamira ya dhati kuhakikisha huduma bora za afya zinasogezwa Jirani na wananchi.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma za mashine ya MRI katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya iliogharimu shilingi bilioni 3. Amesema kusogezwa kwa huduma bora kama uwepo wa MRI katika hospitali hiyo ni lengo la kuwapunguzia wananchi gharama na adha za kufuata huduma hizo maeneo ya mbali.

Makamu wa Rais ameupongeza uongozi na wahudumu katika hospitali hiyo kwa kuendelea kujitoa katika kuwahumia wananchi na ubunifu walioufanya katika kutafuta vifaa mbalimbali ikiwemo vya kusafirisha wagonjwa ndani ya hospitali.

Aidha ametoa wito kwa uongozi wa hospitali ya rufaa ya kanda Mbeya kuzingatia utunzaji wa MRI hiyo ikiwemo kuzingatia muda maalumu wa matengenezo uliopangwa ili itoe huduma kwa muda mrefu.

Pia ameagiza Wizara ya Afya kukamilisha utaratibu unaopaswa ili kuifanya Hospitali hiyo kuwa taasisi na kujiendesha kiufanisi zaidi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema wabunifu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya wako katika hatua za mwisho kutengeneza kifaa maalum kinachowekwa mkononi kwa mgonjwa kitakachoweza kutuma ripoti kwa daktari muda wote hali ya hali ya mgonjwa inavyobadilika hata akiwa mbali na hospitali.

Amewapongeza wabunifu katika hospitali hiyo kwa kutumia rasilimali ziliozopo kubuni masuluhisho mbalimbali kwa lengo la kutoa huduma bora hospitalini. @dr_philip_isdor_mpango @ofisi_ya_makamu_wa_rais

Read More