Browsing: Video Mpya

Tanzania inajivunia utajiri mkubwa wa bayoanuai ikiwa na hekta milioni 48.1 za misitu, sawa na asilimia 51 ya eneo la nchi kavu, ambayo ni makazi ya viumbe na vyanzo vya maji vinavyosaidia ustawi wa maisha na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Rodrick Mpogolo, alipozindua Programu Atamizi ya Ujasiriamali wa Mazingira Tanzania chini ya Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai.

Mradi huu unaofadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) unalenga urejeshaji wa hekari 110,000 za maeneo ifikapo mwaka 2025 na unatekelezwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Makamu wa Rais, UNEP, na IUCN katika Halmashauri saba za mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa, na Njombe.

Wajasiriamali 42 kati ya 46 wameanza mafunzo ya ujasiriamali wa kimazingira, wakijikita katika kilimo endelevu, ufugaji nyuki, nishati safi, na urejelezaji wa taka.