*DKT. TULIA AMUOMBA RAIS SAMIA KUBORESHA MIUNDOMBINU JIJINI MBEYA*
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameiomba Serikali kupitia kwa Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuboresha barabara chakavu za mitaa ya Jimbo hilo ambazo ni zaidi ya km 400.
Dkt. Tulia ameyasema hayo wakati wa kilele cha Maonesho na sherehe za wakulima nanenane kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya leo tarehe 8 Agosti, 2023.
Pamoja na ombi hilo, Dkt. Tulia amemshukuru Rais Dkt. Samia na Serikali yake ya awamu ya sita kwa kufanikisha uboreshwaji wa sekta mbalimbali katika Jiji hilo ikiwemo elimu, afya na zaidi kutoa Shilingi Trilioni 1.1 kwa ajili ya kujenga barabara ya njia nne kutokea Igawa hadi Tunduma yenye urefu wa KM 218.
Kuhusu uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Dkt. Tulia amemueleza Rais Dkt. Samia kwamba Wananchi wa Jiji la Mbeya wamemuagiza amueleze kwamba wameukubali na kuubariki uwekezaji huo wenye maslahi mapana kwa taifa.
Akijibu ombi hilo, Rais Dkt. Samia ameahidi kwenda kujipanga na Serikali yake ili kuona namna ambayo wataweza kufanya maboresho hayo ya barabara za mitaa ya Jiji hilo.