Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi Julai 1,2025 amefungua kambi ya matibabu bila gharama kwa wagonjwa wa macho Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya inayolenga kuwafikia wagonjwa zaidi ya mia mbili.
Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema gharama zote za uchunguzi,dawa na matibabu ni bure kupitia wadau wake kutoka Ujerumani na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.
Dkt Fariji Kilewa Mkuu wa Kitengo cha macho Hospitali ya Mkoa wa Mbeya amesema lengo ni kuwafikia wagonjwa zaidi ya mia mbili waliopo Mkoa wa Mbeya na mikoa jirani.
Aidha amesema mbali ya upasuaji wa mtoto wa jicho pia wanawafanyia uchunguzi wa macho kwa matatizo mengine ya macho.
Hata hivyo Dkt Fariji Kilewa amesema gharama za upasuaji wa mtoto wa jicho zinagharimu zaidi ya shilingi laki tatu ambazo ni watu wachache wanaoweza kumudu gharama hizo.
Afisa uhusiano Hospitali ya Mkoa wa Mbeya Agrey Mwaijande amesema gharama zote zinatolewa bure hivyo wito umetolewa kwa wananchi kuitumia vizuri fursa hiyo.
Baadhi ya wagonjwa waliojitokeza kupatiwa watibabu wamepongeza huduma hiyo kutokana na wengi wao kushindwa kumudu gharama za matibabu ya macho.
Hii ni kambi ya pili kwa Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi kuandaa kambi ya macho iliyoanza juni 30,2025 itakayotamatika julai 5,2025kwa ushirikiano na Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.