Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari Wanyama pori [TAWA] kutoka Mpanga Kipengele linamshikilia Frank Alon [49] mkazi wa Uyole – Nsalaga Jijini Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali meno nane [08] ya Tembo yenye uzito wa kilogram 31.6 bila kibali.
Mtuhumiwa alikamatwa Agosti 17, 2025 saa 9:00 alasiri Kijiji cha Nsonyanga kilichopo Kata ya Mahongole, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali katika muendelezo wa Misako na Doria za pamoja zinazofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari Wanyama Pori [TAWA].
Mtuhumiwa alikuwa akisafirisha meno hayo ya Tembo kwa kutumia usafiri wa Pikipiki yenye namba za usajili MC 165 DDF aina ya TVS akiwa katika harakati za kutafuta mteja. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa ni mwindaji haramu katika hifadhi za Taifa.