Dkt. David Nassoro, Daktari Bingwa Mbobezi wa Mishipa ya Fahamu, amefafanua kuhusu magonjwa mawili yanayozua changamoto kubwa katika jamii – Kiharusi kinachowakumba zaidi watu wazima, na Degedege linaloathiri watoto wadogo.
Akieleza kwa undani, Dkt. Nassoro amesema Kiharusi hutokana na kuziba au kupasuka kwa mishipa ya damu kwenye ubongo.
“Dalili za awali ni muhimu kuzitambua. Mgonjwa akipata ganzi upande mmoja, kushindwa kuongea au kuona, lazima apelekwe hospitali haraka – ndani ya saa tatu tuna nafasi kubwa ya kuokoa maisha,” amesema.
Kwa upande mwingine, Degedege limekuwa tatizo linalowachanganya wazazi, wengi wakidhani ni uchawi. Lakini Dkt. Nassoro amesisitiza kisayansi kuwa chanzo kikuu ni homa kali, hasa malaria.
“Wazazi wanapaswa kuelewa kuwa mtoto akianza kutetemeka, kupoteza fahamu kwa muda, au kuvuja mate, wanapaswa kumpeleka hospitalini mara moja. Kukaa nyumbani au kutegemea tiba zisizo sahihi kunaongeza hatari,” ameongeza.
Akihitimisha, Dkt. Nassoro amesema kinga ni hatua ya kwanza, ikiwemo kuzingatia lishe bora, kupunguza msongo wa mawazo, kufanya mazoezi, na kwa upande wa watoto kutumia vyandarua vyenye dawa ili kujikinga na malaria.
“Elimu kwa jamii ndiyo tiba ya kwanza. Tukiepuka imani potofu na kuzingatia huduma za kitabibu, tunaweza kuokoa maisha ya maelfu ya Watanzania,” amesema Dkt. Nassoro.