Mbeya, Septemba 5, 2025 — Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Dkt. Tulia Ackson, ametoa wito kwa vijana nchini kutumia michezo, hususan mpira wa miguu, kama njia ya kujipatia ajira na kuboresha maisha yao.
Dkt. Tulia alitoa kauli hiyo leo wakati wa tamati ya mashindano ya Tulia Trust Uyole Super Cup yaliyofanyika mkoani Mbeya, ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Amesema michezo ni sekta yenye fursa nyingi, ikiwemo ajira, na hivyo vijana wanapaswa kujituma, kuwa na nidhamu, na kuendeleza vipaji vyao ili kufanikisha malengo yao.
Aidha, Dkt. Tulia amethibitisha kuwa taasisi yake ya Tulia Trust itaendelea kudhamini mashindano hayo kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, kwa lengo la kuibua na kukuza vipaji vya vijana pamoja na kuendeleza michezo nchini.