Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, ametangaza kuwa Mkoa wa Mbeya umepewa heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mhe. Malisa amesema maandalizi yote ya sherehe hizo yanaendelea kwa kasi ili kuhakikisha Mkoa wa Mbeya unakuwa mwenyeji bora na unatimiza matarajio ya kitaifa.
Amesema sambamba na sherehe hizo, Mkoa wa Mbeya utakuwa na matukio mbalimbali ikiwemo:
Maonyesho ya Wiki ya Vijana yatakayofanyika kuanzia tarehe 08 – 13 Oktoba, 2025 katika Uwanja wa Soko la zamani Uhindini.
Misa Maalum ya Kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere itakayoadhimishwa tarehe 14 Oktoba, 2025 katika Kanisa Katoliki la Mwanjelwa.
Kupokelewa kwa Mwenge wa Uhuru utakaopokelewa na Mkoa wa Mbeya kutoka Mkoa wa Songwe kuanzia tarehe 07 – 13 Oktoba, 2025.
Sherehe za Kilele cha Kitaifa cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba, 2025.
Wito kwa Wananchi na Wadau
Mhe. Malisa ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya kujitokeza kwa wingi kushiriki sherehe hizo muhimu za kitaifa, hususan wakati Mwenge wa Uhuru unapita katika maeneo mbalimbali ya Mkoa.
Ameeleza kuwa ni muhimu wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kilele ili kuujaza uwanja na kusherehekea tukio hilo la kihistoria.
Vilevile, ameyataka vyombo vya habari kuendelea kutoa taarifa kwa wananchi ili kudumisha mshikamano, amani na umoja katika Mkoa wa Mbeya na taifa kwa ujumla.
Aidha, amewataka wamiliki wa hoteli na nyumba za kulala wageni kuandaa maeneo ya malazi ya kutosha kwa wageni wote watakaoshiriki, huku akiwataka kutoongeza gharama za huduma hizo.
Wafanyabiashara wa vyakula na usafirishaji pia wamehimizwa kujipanga kwa ajili ya kutoa huduma bora kutokana na wingi wa wageni watakaofika Mbeya kwa ajili ya sherehe hizo.
Hitimisho
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, amesisitiza kuwa Mkoa wa Mbeya umejipanga kikamilifu na upo tayari kwa heshima ya kuandaa kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025.
“Mbeya ipo tayari kwa ajili ya kilele,” amehitimisha.