Kijana Golden Kidumba, maarufu kama DON. G, amewagusa watoto wa mitaani kwa kuwapatia chakula, kuwanunulia nguo na kutumia muda wa siku nzima akiwa nao, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuikumbuka jamii aliyotokea.
Golden, mzaliwa na mkazi wa zamani wa Njombe, anasema maisha magumu aliyoyapitia utotoni ndiyo yamemfanya kuwa na moyo wa huruma na kujitoa kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.
“Nimekulia kwenye maisha magumu sana. Lakini namshukuru Mungu kwa kunibariki na kunifanya niweze kuwakumbuka hawa wadogo zangu wa mitaani. Nimekula nao, nimesherehekea nao na pia nimewanunulia nguo ili wajisikie wanathaminiwa kama watoto wengine,” amesema DON. G.
Amesema kusaidia watoto wa mitaani si tukio la leo pekee, bali ni jambo alilolianza miaka kadhaa iliyopita, ikiwemo kutembelea hospitali na kuwasaidia watu wenye uhitaji.
Golden ameweka wazi kuwa ndoto yake ya baadaye ni kuanzisha taasisi ya msaada na hata kujenga shule maalum kwa ajili ya watoto hao, ili kuwapa elimu, malezi na fursa za kuanza maisha mapya.
Baadhi ya watoto wa mitaani waliopokea msaada huo wameeleza machungu ya maisha yao, ikiwemo vipigo, njaa, manyanyaso na mara nyingi kudharauliwa kama wahalifu bila kujua historia zao.
Kijana Brian Edwin, anayelelewa katika kituo cha Mtama, amesema:
“Maisha ya mitaani ni magumu. Tunapigwa, tunanyanyaswa na tunaishi bila uhakika. Lakini leo tumepata faraja kubwa kutoka kwa DON. G. Mungu ambariki.”
Wengine kama Anody Nyondo na Gifty wameeleza jinsi walivyokimbia nyumbani kutokana na migogoro ya kifamilia na manyanyaso, hali iliyowalazimu kuingia mitaani.
Watoto hao wameiomba jamii na serikali kutowatenga, bali kuwaona kama watoto wanaohitaji msaada na si wahalifu.
Golden ameendelea kutoa wito huo huo:
“Tusishikilie mali bila sababu. Tukiondoka duniani, hatuchukui chochote. Tuwakumbuke watoto wa mitaani; wanahitaji upendo na msaada wetu.”

