MAMIA WAMPOKEA DKT. SAMIA ARUSHA, ASISITIZA UMUHIMU WA AMANI NCHINI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewashukuru wananchi wa Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kwa imani kubwa waliyompatia katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akiahidi kurejea tena Mkoani Arusha kutoa shukrani zake kwa wananchi.
Dkt. Samia amebainisha hayo leo Ijumaa Novemba 21, 2025 alipotua katika Uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) na kuzungumza na mamia ya wananchi waliofika uwanjani hapo Kumpokea, akianza ziara yake ya siku mbili Mkoani Arusha.
Katika salamu zake Rais Samia amesisitiza kuhusu umuhimu wa amani kwa ustawi na maendeleo ya Watanzania, akisisitiza wananchi kutotoa fursa katika kuharibu amani na kuwasihi Wazazi na walezi kuzungumza na Vijana wao pia kuhusu umuhimu wa kutunza amani ya Tanzania.
“Niwashukuru sana kwa kuendelea kuiweka mikoa hii kuwa salama. Usalama upo, kazi zinaendelea na mambo yetu yote yanaendelea. Niwaombe sana amani pekee ndiyo tumaini letu, uhai wetu ni amani yetu sasa niwaombe sana tusitoe fursa ya kuharibu amani yetu.” Amesema Rais Samia.
Rais Samia pia ametoa wito kwa wazazi na walezi kuzungumza na watoto wao kuhusu amani, akisema anafahamu kuwa matukio ya uvunjifu wa amani ya Oktoba 29, 2025 Vijana wengi walifuata mikumbo, akisema ni muhimu kuilinda amani kwani masuala ya uvunjifu wa amani si masuala ya kufanyia majaribio nchini.
Rais Samia yupo Mkoani kwa ziara ya siku mbili ambapo kesho Jumamosi Novemba 22, 2025 anatarajiwa kutunuku Kamisheni na Shahada ya Sayansi ya Kijeshi kwa Maafisa wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli Mkoani Arusha.

