Miaka kadhaa nyuma, aliishi kijana mmoja aitwaye Oscar, mkazi wa Songwe, kijana mwenye ndoto kubwa na moyo wa kutokata tamaa. Oscar alikulia katika familia ya kawaida, lakini wazazi wake walifanya kila wawezalo kuhakikisha anapata elimu bora. Alipata bahati ya kusoma hadi Chuo Kikuu, ambako alisomea masuala ya biashara na utawala. Alifaulu kwa kiwango cha juu sana, jambo lililompa matumaini makubwa kuwa baada ya kutoka chuoni angepata kazi haraka na kuanza kujenga maisha yake.
Lakini maisha yalipomkumba, hakutarajia changamoto alizokutana nazo. Mwaka wa kwanza baada ya kuhitimu ulipita bila mafanikio. Alipeleka maombi ya kazi katika kampuni zaidi ya hamsini, lakini kila mara taarifa zilikuwa zilezile: “Tunasikitika kukujulisha kwamba hukufanikiwa…” Mwaka wa pili nao ukapita vivyo hivyo. Wakati marafiki zake wakiendelea mbele na kazi nzuri mijini, Oscar aliendelea kukaa nyumbani, akifanya vibarua vidogo ili angalau apate hela ya kujikimu.
Kijana huyo aliyekuwa mchangamfu alianza kupoteza matumaini. Alianza kuhisi kama dunia imemsahau. Kila asubuhi aliamka akipitia tovuti za kazi, akituma maombi mapya, lakini jioni zilimkuta akivunjika moyo. Wakati mwingine alijihisi kama elimu yake haina maana tena. Familia yake ilimfariji sana, lakini hata wao waliweza kuona jinsi ambavyo kijana wao alianza kulemewa na mawazo. Soma zaidi hapa

