Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, ametunuku Shahada kwa wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Mbeya, katika Mahafali ya 24 yaliyofanyika leo, tarehe 27 Novemba 2025.
Akizungumza katika mahafali hayo, Dkt. Shein amewataka wahitimu kuwa na nidhamu, uadilifu, na bidii ya kazi wanapoingia kwenye soko la ajira na katika nafasi zao za kulitumikia taifa. Ameeleza kuwa dunia ya sasa inahitaji viongozi na wataalamu wanaojituma, wabunifu, na wenye maadili mema.
Amesisitiza kuwa elimu waliyoipata Mzumbe ni nguzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya nchi, hivyo ni wajibu wa kila mhitimu kujiandaa kikamilifu na kutumia taaluma yao kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
Mahafali hayo yamehudhuriwa na viongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe, wadau wa elimu, wazazi, na ndugu wa wahitimu kutoka maeneo mbalimbali.

