kuu wa Mkoa wa Mbeya, Benno Malisa, amewataka watumishi wa taasisi za serikali Nyanda za Juu Kusini kulinda kwa wivu rasilimali za taifa kwa kutumia ipasavyo maendeleo ya teknolojia, ili kutimiza adhima ya serikali ya kupata thamani halisi ya fedha katika manunuzi ya umma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Mfumo wa NesT, yanayojumuisha moduli mpya za majadiliano, uandaji na usimamizi wa mikataba, Malisa amesema usimamizi usioridhisha wa mikataba ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazokwamisha upatikanaji wa thamani ya fedha katika ununuzi wa umma.
Amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali yataongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika michakato ya ununuzi, sambamba na kupunguza mianya ya upotevu wa fedha za umma.
Kwa upande wake, Meneja wa PPRA Nyanda za Juu Kusini, Pascal Manono, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuweka uwazi katika hatua zote za ununuzi, kuanzia mchakato wa zabuni hadi usimamizi wa mikataba, kwa kutumia moduli mpya zilizoboreshwa ndani ya mfumo wa NesT.
Nao washiriki na wawezeshaji wa mafunzo hayo wamesema kuwa uelewa walioupata kuhusu matumizi ya moduli mpya utawasaidia kuboresha utendaji kazi wao na kutoa huduma kwa wananchi kwa weledi, ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji.

