#MbeyaYetuTv
Serikali inaendelea kujenga jengo kubwa la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe (SIA) uliopo katika kata ya Bonde la Songwe jimbo la Mbeya vijijini ikiwa ni mkakati wake wa kuboresha sekta ya usafiri wa anga ikiwemo kuweka mazingira rafiki kabla na baada ya abiria kusafiri kutoka na kwenda nchi mbalimbali.
Akitoa taarifa kwa kamati ya siasa ya halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbeya vijijini (Kichama) kwenye ukaguzi wa mradi huo Kaimu Meneja wa wakala wa barabara Tanzania TANROADS Mhandisi Joel Samwel Mwabungu alisema ujenzi huo unatekelezwa na serikali kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni 14 na wanatarajia kukamilisha jengo hilo kufikia march 2023.
Kuhusu uwekaji taa za kuongozea ndege kiongozi huyo alisema tayari zilishakamilika na zinatumika vizuri hivyo ndege zinaweza kutua na kuanza safari usiku na mchana.
Wajumbe wa kamati ya siasa akiwemo Danieli Kapusi, Willium Simwali na Subiraga Mwangoka walieleza kuridhishwa kwao na utekelezwaji miradi mbalimbali kwenye uwanja huo katika kupanua wigo wa kuwahudumia wasafiri.
Michael Ngailo ni Diwani wa Kata ya Bonde la Songwe ulipo uwanja wa ndege wa Songwe alisema uwanja huo umekuwa na faida kwa jamii isipokuwa changamoto ni wanafunzi wa eneo la Iwejele kuzuiliwa kupita kwenye eneo la uwanja kwenda shuleni baada ya mamlaka kujenga uzio kuzunguka uwanja huo na kuiomba serikali kupitia wizara ya uchukuzi kutekeleza ahadi zao kwa wananchi wa Kata ya Bonde la Songwe Mbeya vijijini.
Msafara wa Kamati ya siasa uliongozwa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbeya vijijini Akimu Sebastian Mwalupindi ambapo baada ya kamati kukagua mfumo wa taa za kuongozea ndege uwanjani hapo na baadaye kukagua jengo la abiria alisema utekelezaji wa ilani ya chama hicho ni wa kiwango cha juu na kinachoridhisha.
Pamoja na hayo CCM wilaya ya Mbeya vijijini kupitia Mwenyekiti Mwalupindi imetumia ziara hiyo ya kikazi kumpongeza Rais Dkt. Samia kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi kuwa Mwenyekiti wa Chama (CCM) Taifa katika uchaguzi wa hivi karibuni.
Pia imempongeza Rais Samia kwa kuendelea kusimamia ipasavyo utekelezwaji miradi mbalimbali nchini katika kuwatumikia wananchi hususani katika sekta za miundombinu ya usafiri, Maji, Afya, Kilimo na Elimu.
Jengo hilo la abiria linajengwa kwa thamani kwa zaidi ya shilingi bilioni 14 na kampuni ya Kichina ambapo pamoja na miradi mingine ya uwanja wa ndege ya Run Ways na taa za kuongozea ndege jumla yake ni zaidi ya shilingi bilioni 30 zitakazotumika katika miradi hiyo.