Browsing: Video Mpya

WANAFUNZI WATANO WAMEFARIKI DUNIA BAADA YA KUGONGWA NA GARI MBEYA.

Tarehe 26.07.2025 saa 11:30 alfajiri huko Kijiji cha Itumba kilichopo Kata ya Chalangwa, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya katika barabara kuu ya Mbeya – Chunya. Gari lenye namba za usajili T.194 DCE aina ya Yutong Bus kampuni ya Safina Coach lililokuwa likitokea Chunya mjini kuelekea Mbeya likiendeshwa na dereva aitwaye Abdul Hassan [28] mkazi wa Mbeya mjini liliwagonga watembea kwa miguu wanafunzi wa Shule ya Sekondari Chalangwa waliokuwa wanakimbia mchaka mchaka (Jogging) na kusababisha vifo vya watu watano.

Waliofariki katika ajali hiyo wametambulika kwa majina ya Seleman Ernest @ msekwa, Samwel Zambi, Kelvin Festo Mwasamba, Hosea Manga Mbwilo na Amina Ndege Ulaya. Aidha, katika ajali hiyo majeruhi ni tisa kati yao saba wamelazwa wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya na Kituo cha Afya Chalangwa ambao ni Benard Mashaka [17], Lilian Raymond [16], Kenedy Masoud [14], Vicent Baraka Malema [17], Siwema Nasibi Simbilo [17], Alex Aules Peter [17], Dethani Adam Charles [15] na wawili ambao wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa ambao ni Getruda Mwakyoma [17], Farida Mwasongole [17].

Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva kushindwa kulimudu gari hivyo kupelekea kwenda kuwagonga wanafunzi waliokuwa wanafanya mazoezi ya kukimbia (Jogging). Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na msako wa kumtafuta dereva wa Basi hilo ambaye amekimbia mara baada ya kusababisha ajali.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa madereva kuwa makini na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Imetolewa na:
Kaimu Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.