Browsing: Video Mpya

Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Mhe. Patrick Mwalunenge, ameendelea kuwawezesha vijana wa bodaboda jijini Mbeya kwa kutoa msaada katika vijiwe mbalimbali.

Katika ziara hiyo, ametoa bodaboda moja kwa vijana wa kijiwe cha Nzovwe, pamoja na mtaji wa mafuta wa shilingi 40,000 kwa kila kikundi alichotembelea. Aidha, ameacha shilingi 400,000 kwa ajili ya kuwaendeleza vijana wengine.

Mhe. Mwalunenge amewahimiza vijana kuwa watulivu na wavumilivu wakati serikali ikiendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha kupitia fursa za kiuchumi.

Wadau wa kilimo kutoka taasisi za Serikali na sekta binafsi wamepatiwa mafunzo juu ya matumizi ya mashine za kisasa za kukaushia na kupima unyevu wa mazao ya nafaka, katika warsha iliyoandaliwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na JICA jijini Mbeya.

Warsha hiyo imefanyika tarehe 26 Novemba 2025 katika shamba la Raphael Group Ltd, ambapo mashine ya Batch Circulating Dryer yenye uwezo wa kukaushia hadi tani 8 za mpunga ndani ya saa 4 imeoneshwa kwa vitendo. Teknolojia hii inatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa upotevu wa mazao baada ya mavuno.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mhandisi Sekela Mwakihaba kutoka Idara ya Zana za Kilimo na Uongezaji Thamani alisema ushiriki wa wadau unaonesha dhamira ya Serikali ya awamu ya sita kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao na kupunguza uharibifu wa nafaka wakati wa uvunaji. Alibainisha pia kuwa Serikali inaendelea kusukuma matumizi ya teknolojia kupitia utekelezaji wa Agenda 10/30 ili kuongeza tija na kipato cha wakulima.

Kwa upande wake, Meneja wa Uzalishaji wa Raphael Group Ltd – Kituo cha Uyole, Bw. Maisha Ambangile, alisema mashine hiyo itasaidia wakulima kupata nafaka kavu kwa ubora wa soko na kwa muda mfupi, huku gharama ya mashine moja ikiwa takriban shilingi milioni 188.

Warsha hiyo imeratibiwa na JICA kwa kushirikiana na kampuni za YAMAMOTO (watengenezaji wa mashine za kukaushia nafaka) na Kett Electric Laboratory (watengenezaji wa mashine za kupima unyevu), ikiwakutanisha maafisa wa Serikali, wataalamu wa JICA, wamiliki wa mitambo ya ukavu na wakulima kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya.

Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, ametunuku Shahada kwa wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Mbeya, katika Mahafali ya 24 yaliyofanyika leo, tarehe 27 Novemba 2025.

Akizungumza katika mahafali hayo, Dkt. Shein amewataka wahitimu kuwa na nidhamu, uadilifu, na bidii ya kazi wanapoingia kwenye soko la ajira na katika nafasi zao za kulitumikia taifa. Ameeleza kuwa dunia ya sasa inahitaji viongozi na wataalamu wanaojituma, wabunifu, na wenye maadili mema.

Amesisitiza kuwa elimu waliyoipata Mzumbe ni nguzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya nchi, hivyo ni wajibu wa kila mhitimu kujiandaa kikamilifu na kutumia taaluma yao kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Mahafali hayo yamehudhuriwa na viongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe, wadau wa elimu, wazazi, na ndugu wa wahitimu kutoka maeneo mbalimbali.