Browsing: Video Mpya

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari Wanyama pori [TAWA] kutoka Mpanga Kipengele linamshikilia Frank Alon [49] mkazi wa Uyole – Nsalaga Jijini Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali meno nane [08] ya Tembo yenye uzito wa kilogram 31.6 bila kibali.

Mtuhumiwa alikamatwa Agosti 17, 2025 saa 9:00 alasiri Kijiji cha Nsonyanga kilichopo Kata ya Mahongole, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali katika muendelezo wa Misako na Doria za pamoja zinazofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari Wanyama Pori [TAWA].

Mtuhumiwa alikuwa akisafirisha meno hayo ya Tembo kwa kutumia usafiri wa Pikipiki yenye namba za usajili MC 165 DDF aina ya TVS akiwa katika harakati za kutafuta mteja. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa ni mwindaji haramu katika hifadhi za Taifa.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Maafisa wa Shirika la Umeme [TANESCO] Tawi la Mbeya linamshikilia Ikupa Mwakibibi [32] mjasilimali na mkazi wa Sae Jijini Mbeya kwa tuhuma za kuhujumu miundombinu ya Shirika la Umeme kwa kujiunganishia umeme kinyume na utaratibu wa shirika hilo.

Mtuhumiwa alikamatwa Agosti 18, 2025 saa 9:30 alasiri Mtaa wa Sae uliopo Kata ya Ilomba Jijini Mbeya katika oparesheni za pamoja za Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Shirika la Umeme [TANESCO] ambapo baada ya kupekuliwa katika nyumba yake mtuhumiwa alikutwa akiwa na mita za umeme 19, rimoti za TANESCO 45 pamoja na waya rola 25 vyote vikiwa ni mali ya shirika la TANESCO.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa saba [09] kwa tuhuma za utapeli na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia mitandao ya kijamii ya Facebook na WhatsApp. Watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti katika Misako inayofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya ambapo Agosti 18, 2025 saa 6:00 mchana huko Kitongoji na Kata ya Nsalala, Tarafa ya Usongwe, walikamatwa watuhumiwa 04 wanaojishughulisha na utapeli wa fedha kupitia mitandao ya Facebook na WhatsApp kwa kudanganya wanatafuta wafanyakazi wa kuuza Supermarket iitwayo Kajala iliyopo Jijini Dar es salaam.

Watuhumiwa waliokamatwa ni Nemia Japhet Njonga [23] fundi rangi, mkazi wa mwakapangala, Ombeni Asangalwisye Ambilikile [22] Bodaboda, mkazi wa Nsalala, Jacob Peter Hamis [23] fundi rangi, mkazi wa mwakapangala, Baraka Joniphat Mgala [22] Bodaboda, mkazi wa mtaa wa Ndola Mbalizi.

Watuhumiwa wamekuwa wakitengeneza link za kughushi kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook na WhatsApp ambapo mtu anayeomba ajira hutumia kujiunga kwenye kundi hilo na kisha hutumiwa ujumbe unaomtaka kutuma CV yake na kumuomba mtume fedha za kujaziwa fomu na kulipia sare za kufanyia kazi. Watuhumiwa wamekutwa wakiwa na simu mbalimbali pamoja na laini za simu za mitandao mbalimbali zilizosajiliwa kwa majina ya watu tofauti ambazo hutumika kupokelea fedha na kufanyia mawasiliano

Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya imepokea vifaa tiba vya kisasa monitor 15 kwa lengo la kuboresha huduma za uangalizi kwa watoto wachanga. Vifaa hivi, vilivyotolewa na Madau wa Maendeleo GOAL 3, vinatarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya kwa watoto wanaohitaji msaada wa haraka na wa kitaalamu.

Akikabidhi vifaa tiba hivyo Mwamvuwa Mika Meneja Mradi Tanzania amesema thamira ya Goal 3 ni hakikisha Watoto wachanga wananzaliwa katika mazingira mazuri na pia wanapata huduma ambayo ni bora.
“Kwa kipindi hiki tumefika hapa hospitali ya rufaa ya kanda Mbeya kwaajili ya kufunga Impala monitors kwenye kitengo cha NIKU ili kuweza kuwasaidia Watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda. Ningependa pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa Uongozi wa hospitali kwasababu tumeweza kushirikiana hadi kwa hatua hii tuliofika leo ambapo tumeshazifunga monitors 15 na zimeshaanza kutoa huduma kwa Watoto walio wodini na pia tutaendelea kushirikiana ili kuwafika Watoto wengine walio kwenye hospitali zingine ” – Mwamvuwa

Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Bi. Myriam Msalale amemshukuru Madau wa maendeleo GOAL 3 kwa kuichagua Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kufanya kazi nayo na kuvipatia vifaa tiba hivyo ambavyo vimekuja kwa wakati na vitatusaidia sana katika kuboresha huduma kwa watoto wachanga na kutoa wito kwa watumiaji wa vifaa tiba hivyo kuvitunza kwa uangalifu wa hali ya juu ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kuwahudumia Watoto waliokuja kupata matibabu.
.

Nae Dkt.Rehema Marando Daktari Bingwa mbobezi wa watoto wachanga, amesema kuwa msaada huo umeleta manufaa makubwa kwa watoa huduma na Watoto ambapo vitawezesha kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa utoaji wa matibabu na uangalizi wa hali ya juu kwa Watoto wachanga.